Thursday, December 14, 2017

Mkutano wa Wataalam kuhusu Mapitio ya Sekta ya Afya - 2017

Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dk. Mpoki Ulisubisya akitoa muongozo wa namna ya uwasilishwaji wa mada mbalimbali katika mkutano wa  Wataalam kuhusu Mapitio ya Sekta ya Afya kwa mwaka 2017 - Technical Review Meeting (TRM). 

Mkurugenzi wa sekta binafsi katika masuala ya afya, Dk. Samwel Ogillo akichangia mada. 


Josephine Nyonyi na Atuswege Mwangomale kutoka Sikika wakifuatilia mjadala wa Mapitio ya Sekta ya Afya kwa mwaka 2017

Mkurugenzi msaidizi anayeshughulikia Afya kutoka Ofisi ya Rais -TAMISEMI Dk. Anna Nswilla akitolea ufafanuzi wa maswali yaliyoulizwa na washiriki mbalimbali katika mkutano wa Mapitio ya Sekta ya Afya kwa mwaka 2017. 

Baadhi ya wadau kutoka mashirika/taasisi mbalimbali ya afya nchini  wakichangia mada, kujadili changamoto, kutoa mapendekezo na kuuliza maswali katika mkutano wa (TRM 2017).
Baadhi ya washiriki wakifuatilia uwasilishwaji wa mada mbalimbali.

Friday, September 22, 2017

Mkutano wa Wadau wa Afya Kigoma

Mkuu wa Ofisi ya Kanda Sikika - Dodoma, Bw. Richard Msittu akitoa utambulisho wa Shirika  kwa Wadau wa Afya katika Mkutano - Manispaa ya Kigoma Ujiji.  

Makamu Meya wa Manispaa ya Kigoma Ujiji, Mh. Athumani Mussa Athumani akitoa neno la ufunguzi.
Mjumbe wa timu ya SAM, Bw. Haji Sangi akiwasilisha hoja mbalimbali za timu ya SAM.  
Wajumbe wa Timu ya Uendeshaji wa shughuli za Afya Manispaa ya Kigoma Ujiji (CHMT) wakifuatalia uwasilishwaji wa mada.
Mganga Mkuu  wa Manispaa ya Kigoma - Ujiji Dk. Peter J. Nsanya akitoa ufafanuzi wa baadhi ya hoja zilizowasilishwa na timu ya SAM. 


Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigoma - Ujiji Bw. Jude Mboya akifafanua baadhi ya hoja zilizowasilishwa katika mkutano huo. 
Mmoja wa wajumbe wa timu ya SAM Bw. Adrophinus Leopold, akichangia maoni. 
Wadau mbalimbali wa afya wakifuatilia uwasilishwaji wa mada katika mkutano huo. 
Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Bw. Kwame Andrew ambaye pia ni mgeni rasmi katika mkutano huo akisoma hotuba kwa niaba ya mkuu wa wilaya hiyo.

Bw. Kwame Andrew akitoa vyeti kwa wajumbe wa timu ya SAM.


Wajumbe wa CHMT wakiwa katika picha ya pamoja na mgeni rasmi (Kaimu mkuu wa wilaya ya Kigoma). 
Makamu Meya, Kaimu Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi wa Manispaa na Wajumbe wa timu ya SAM  Kigoma - Ujiji wakiwa katika picha ya pamoja. 

Thursday, August 3, 2017


Pongezi Serikali kwa Hatua Kuimarisha Upatikanaji Dawa
... iboreshe mifumo kuongeza upatikanaji

Mara kwa mara, tumekuwa tukitoa matamko na mapendekezo ili kuboresha upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi, hususan dawa na vifaa tiba.  Kwa ujumla, hali ya upatikanaji wa dawa nchini inaanza kuimarika ingawa bado kuna baadhi ya changamoto ambazo tuna imani zinaweza kushughulikiwa.

Ufuatiliaji wa Sikika uliofanyika kupitia mahojiano na wananchi waliotoka kupata huduma za afya, asilimia 81 ya waliohojiwa  mwaka 2017 waliweza kupata dawa zote walizoandikiwa ukilinginisha na asilimia 51 ya wananchi waliohojiwa mwaka 2016 (ongezeko la asilimia 30). Ufuatiliaji huu ulifanyika katika wilaya ambazo Sikika inafanya kazi. Sikika inaipongeza serikali kwa hatua inazochukua katika kuimarisha upatikanaji wa dawa nchini hasa ikikumbukwa kwamba:

Kwanza, kulikuwepo malalamiko juu ya gharama za baadhi ya dawa zinazosambazwa na Bohari Kuu ya Dawa nchini, (MSD) kulinganisha na za wauzaji binafsi. Suala hili limefanyiwa kazi kwa kiasi kikubwa kwa kuanzisha utaratibu wa kuagiza dawa moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji, viwandani. Kwa mujibu wa  Wizara ya Afya,  Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (MOHCDGEC), utaratibu huu umepunguza gharama za  dawa kwa kati ya asilimia 15 hadi 80, hivyo kuongeza upatikanaji wa dawa vituoni, kwa gharama nafuu.

Pili, kwa miaka miwili mfululizo kumekuwa na ongezeko la bajeti ya dawa ambayo ni hatua nzuri kwa serikali katika kuboresha huduma za afya. Fedha zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya dawa kwa mwaka wa fedha 2016/17, (Tsh bilioni 251) zilitolewa kwa kiasi kikubwa (Tsh bilioni 132) ikilinganishwa na mwaka wa fedha 2015/16 ambapo zilitengwa Tsh bilioni 31 na kutolewa Tsh bilioni 24. Hatua hii imeiongezea MSD uwezo wa kuagiza na kununua dawa, na hivyo kuongeza upatikanaji wake vituoni.

Tatu, kwa miaka kadhaa Sikika  imekuwa ikiishauri serikali iondoe ukiritimba wa MSD kuwa sehemu pekee ambapo vituo vinatakiwa kununua dawa. Hii imekuwa ikisababisha matatizo pale ambapo dawa husika hazipatikani MSD na vituo haviruhusiwi kununua sehemu nyingine hata kama vina fedha. Kwa sasa, vituo vya huduma vimeruhusiwa kununua dawa kutoka kwa wauzaji binafsi pindi zinapokosekana MSD.

Tumefurahishwa na mipango ya maboresho na mgawanyo wa majukumu kati ya  MOHCDGEC na TAMISEMI katika kusimamia utoaji wa huduma za afya ikiwemo  upatikanaji wa dawa vituoni. Utawala wa vituo vya afya na idara za afya katika halmashauri umeimarika zaidi.

Pamoja na pongezi hizi, kuna changamoto kadhaa ambazo tungependa kuona serikali ikiendelea kuzifanyia kazi.

·      Kwanza, MSD iimarishe mawasiliano na wadau, hususan kwa kutoa taarifa muhimu ili kuimarisha ufuatiliaji na uwajibikaji katika mfumo wa ugavi. Mfano, kutoa taarifa za upatikanaji wa dawa kupitia tovuti yao kama ilivyokuwa awali.

·      Pili, MSD kuwa mnunuzi na msambazaji pekee wa dawa bado ni changamoto kwasababu nchi ni kubwa kijiografia na vituo vya huduma ni vingi (zaidi ya 5000). Hivyo basi tunapendekeza kwamba MSD isiwe mshitiri pekee. Kwa Mfano, ongezeko la sasa la upatikanaji wa dawa vituoni haukutokana na MSD pekee bali pia uwezo wa vituo kukusanya fedha na kununua dawa kutoka kwa wauzaji binafsi.

·      Tatu, kumekuwa na changamoto kwenye upatikanaji wa vifaa na vifaatiba  katika vituo vingi vya huduma vya afya na hivyo wagonjwa kupewa rufaa zisizo za lazima. Serikali iwekeze katika kununua vifaa hivyo na kukarabati vilivyopo ili kuongeza ubora wa huduma.

·      Nne, kumekuwa na malalamiko kwamba baadhi ya dawa katika baadhi ya vituo zinapotea. Serikali  iweke mifumo imara ya kudhibiti  upotevu wa dawa vituoni. Mfumo ulioanzishwa wa kielektroniki wa kuendesha hospitali (GoT-HoMIS) ukisimikwa vituo vyote nchini utaweza kusaidia kupunguza tatizo hili.

Irenei Kiria
Mkurugenzi Mtendaji- Sikika, SLP 12183 Dar es Salaam,
Simu: +255 222 666355/57, Fax: 2668015, B/pepe: info@sikika.or.tz, Tovuti: www.sikika.or.tz
Twitter: @sikika1, Facebook: Sikika Tanzania, Instagram: sikikatanzania