TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI, MAY 10, 2013
Tumesikitishwa na kauli iliyotolewa bungeni
na Mh. Zarina Madabida, mbunge wa viti maalum, mnamo Mei 8, 2013 akidai
kwamba Sikika imekuwa ikiwakusanya wagonjwa ambao wanaishi na virusi vya UKIMWI
(WAVIU) na kuwachochea waandamane kwenda ofisi za Chama cha Mapinduzi (CCM).
Tumesikitishwa zaidi na kitendo cha Bunge kuruhusu baadhi ya wabunge kutumia
muda wa Bunge kutetea maslahi yao binafsi badala ya taifa.
Mh. Madabida
alitoa tuhuma hizo wakati wa kipindi cha Bunge alipokuwa
akichangia bajeti ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa mwaka wa fedha 2013/14.
Mh. Madabida alinukuliwa akisema “…Sikika
imekuwa inawakusanya wagonjwa ambao wanaishi na virusi vya UKIMWI na kuwaleta
mjini Dar-es-Salaam ili waandamane kwenda CCM… Lakini wamekuwa wakifanya
uchochezi na kwenda ofisi moja hadi nyingine kwenda kufuata hizi habari…” Mh.
Madabida ni mmoja wa wamiliki wa kiwanda cha Tanzania Pharmaceutical Industries
(TPI), ambacho hivi karibuni kimetuhumiwa kuzalisha ARVs bandia na kuiuzia MSD.
Hata hivyo,
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Mh. Hussein Mwinyi aliliambia Bunge tarehe 9
Mei kwamba ana uhakika kabisa kuwa TPI haihusiki kutengeneza dawa hizo, ingawa
taarifa rasmi ya uchunguzi kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DPP)
haijatolewa kwa umma hadi leo. Awali, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii
iliwasisitizia Watanzania kwa nyakati tofauti kwamba ina ushahidi kuwa dawa
hizo bandia za ARVs zilitengenezwa na TPI. Kufuatia msisitizo huo, Wizara ilitoa
amri ya kufunga kiwanda cha TPI.
Sikika inatamka wazi na kukanusha kwamba haijawahi hata mara moja kuomba kibali au kuratibu maandamano yoyote
ambayo kwa njia moja au nyingine yaliwahusisha WAVIU na kuwapeleka kwenye ofisi
za CCM kama alivyoeleza Mh. Zarina Madabida bungeni. Taarifa alizotoa Mh.
Madabida si za kweli na zinalenga kuchonganisha na kuharibu muonekano wa
Shirika kwa jamii ya watanzania wanaofaidika na shughuli au tafiti mbalimbali
zinazofanywa na Sikika. Pia, hakuna mantiki wananchi kuandamana kwenda ofisi za
CCM kwa kadhia ya ARVs bandia kwani wahusika wa kadhia hii ni Wizara ya Afya na
Polisi. Kwa hiyo, kauli ya Madabida inatia shaka kuhusu ufahamu wake wa mambo
labda kama alikusudia tu kuihusisha CCM ili apate huruma ya chama na ili kimtetee.
Sikika
ni shirika lisilo la kiserikali lililosajiliwa nchini Tanzania kwa lengo la
kufanya utetezi juu ya utawala na upatikanaji wa huduma bora za afya kwa
watanzania wote ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa dawa zenye ubora na viwango
halali. Kwa hiyo, Sikika ingekiuka mojawapo ya malengo ya kuandikishwa kwake
kama isingefuatilia sakata la ARVs bandia kwa sababu tu mojawapo ya wamiliki wa
kiwanda kinachotuhumiwa ni Mbunge au kada wa chama cha siasa.
Kwa
malengo hayo, Sikika itaendelea kutetea kwa kadri iwezavyo, bila upendeleo wala
uonevu na kuhakikisha kuwa watanzania wote, wakiwemo WAVIU wanapata huduma bora
za afya ikiwemo dawa na vifaa tiba ambavyo havina athari kwa afya zao. Kwa kuwa
afya na uhai wa baadhi ya watanzania waliotumia hizo ARVs bandia zilihujumiwa,
Sikika inaamini kwamba haki zao zilikiukwa. Hivyo tutafuatilia sakata hili hadi
ukweli uwekwe wazi na wahusika wachukuliwe hatua. Hata kama itagundulika kuwa
wahusika hao ni Wabunge, makada wa vyama au watendaji wa serikali.
Tunapendekeza
Bunge letu liendelee kusimamia ukweli daima na kuhakikisha kuwa taarifa zinazotolewa
na mbunge yeyote ni za kweli na hazilengi kuchafua watu binafsi ama taasisi ambazo
hazina fursa ya kujitetea ndani ya Bunge hilo. Hivyo basi, Sikika inamtaka Mh.
Madabida kuthibitisha tuhuma hizo au sivyo aombe radhi kwa shirika.
Tunawakumbusha
wabunge kwamba Bunge linaendeshwa kwa kodi za wananchi, hivyo litumike kutetea
maslahi ya watanzania wote badala ya kutumika kama sehemu ya kulinda na kutetea
maslahi binafsi. Michango yote ya kuongea ya Mh. Zarina Madabida Bungeni katika
bajeti ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ilikuwa inalenga kutetea ama
maslahi yake binafsi au maslahi ya kiwanda cha TPI ambacho yeye ni mmoja wa
wamiliki.
Bw. Irenei Kiria
Mkurugenzi Mtendaji, Sikika, S. L. P 12183 Dar es Salaam,
Simu: +255 222 666355/57, Nukushi: 2668015, Barua
pepe: info@sikika.or.tz, Tovuti: www.sikika.or.tz
No comments:
Post a Comment