Kwanza tunapenda kuipongeza Tume ya Katiba kwa kazi kubwa
waliyofanya katika kukusanya maoni na kuandaa rasimu ya pili ya Katiba na
vilevile kwa kugusia Afya katika Haki za binadamu kwa baadhi ya makundi kama vile
katika Haki ya wanawake Ibara ya (47) kifungu cha 1(g) mwanamke ana haki ya kupata
huduma bora ya Afya, katika Haki ya watoto Ibara (43) kifungu cha (1)e kinachosema
mtoto ana haki ya kupata lishe bora, huduma ya Afya, makazi na mazingira
yanayomjenga kimaadili.
Hata hivyo, tunasikitika kwamba Haki ya Afya haijatambuliwa kwenye rasimu kama haki ya Msingi ya kila
mwananchi. Tukiwa kama wadau wa Afya, tunapenda kufafanua kuwa Afya ni kuwa
mzima kiakili, kimwili, kijamii, kimaadili na kimazingira, hivyo Afya ni haki
ya msingi ya kila mwananchi. Mwananchi anapokosa haki hii ya msingi hushindwa
kushiriki katika shughuli mbalimbali za kuleta maendeleo, na kupata madhara mengine
yanayoweza kusababisha kifo.
Katika rasimu ya pili ya Katiba iliyokabidhiwa kwa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ajili ya kujadiliwa katika Bunge la Katiba Februari
2014, Afya kama Haki ya msingi ya binadamu haijatambuliwa kama vile haki
zingine zilivyotambuliwa kwa mfano elimu.
Tunatambua kwamba Katiba ndiyo sheria Mama, hivyo basi, pasipo
kutambua Haki ya Afya, sheria ndogondogo haziwezi kulitambua suala hili nyeti,
na hivyo kuiweka jamii na vizazi vijavyo katika hali hatarishi kiafya.
Juni 2013, Sikika iliomba na hatimaye ikapata kibali rasmi
kutoka Tume ya mabadiliko ya Katiba cha kutambuliwa kama Baraza la Katiba kwa
ajili ya kuchambua na kukusanya maoni juu ya Rasimu ya Katiba. Sikika
ilishirikisha wananchi na Asasi mbalimbali kama Tanzania Public Health Association (TPHA), Medical Association of Tanzania (MAT) na Kituo cha Sheria na Haki za
Binadamu (LHRC) katika kuchambua
rasimu ya kwanza ya Katiba na hatimaye kutoa mapendekezo ya kutambua haki ya
afya kwenye Katiba. Mapendekezo hayo yaliwakilishwa kwa Tume Agosti 2013 lakini
hayakuchukuliwa, kwa sababu moja au nyingine.
Kutokana na umuhimu wa Afya kwa kila mwanadamu, tunapendekeza
Afya itambulike kama Haki ya msingi
katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na iwe ni wajibu wa kila
mwananchi kutunza Afya yake, kushiriki na kusimamia masuala yanayohusu afya ya
jamii. Pia serikali ya Jamhuri ya Muungano, mamlaka za nchi pamoja na taasisi
zihakikishe kuwa Haki hii ya msingi inasimamiwa vyema. Pia itambuliwe kuwa ni
kosa la jinai kwa mwananchi kufanya tendo lolote linalohatarisha afya ya mtu
mwingine na jamii kwa ujumla.
Pia tunaomba serikali na wadau wa Katiba waangalie na kutambua Afya kama suala la msingi
linalotakiwa lizingatiwe katika sera zote za maendeleo ili kuweza kulinda afya
ya Watanzania wote.
Aidha, tunapendekeza ibara ya 41 inayozungumzia uhuru na haki
ya mazingira safi na salama iongeze masuala haya; (1) Serikali ihakikishe kuwa kila mwekezaji
afanye tathmini ya kiafya kabla mradi haujaanza na utekelezaji wa mapendekezo
ushirikishe wadau wote hususan, ngazi ya jamii. (2) Serikali na vyombo husika
vidhibiti uingizwaji na utumiaji wa vifaa/vyakula/madawa vyenye viwango duni na
pia kutoruhusu matumizi ya madawa au vyakula bila ya ushahidi wa kitafiti
unaothibitisha usalama wa mtumiaji/mlaji. Kutompatia mwananchi haki ya afya ni
sawa na kumnyima haki ya kuishi kama ilivyoainishwa katika ibara 24 ya rasimu
ya Katiba, maana uhai we mtu unategemea afya aliyo nayo.
Tunaamini kwamba bado kuna nafasi ya kuitambua Afya kama Haki ya msingi, hivyo tunatoa
wito kwa Wajumbe, Viongozi na Wabunge wazingatie suala hili wakati wa kuijadili
rasimu ya Katiba katika Bunge la Katiba.
Tamko hili limeandaliwa kwa ushirikiano kati ya
Sikika, Tanzania Public Health Association (TPHA), Medical association of
Tanzania na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).
No comments:
Post a Comment