Monday, October 8, 2012

Taarifa Kwa Umma

Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko zinatakiwa kuhakikisha kuwa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) pamoja na Shirika la Viwango nchini (TBS) wanachukua hatua za haraka katika kuteketeza bidhaa zote ambazo hazina ubora zilizotajwa hivi karibuni katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa Wabunge.

Ripoti hiyo ilitaja baadhi ya bidhaa zisizokuwa na ubora ambazo zinaweza kuwa katika mzunguko wa soko huku TBS ikiwa ina ufahamu. Baadhi ya bidhaa hizo ni pamoja na vinywaji vya kuongeza nguvu, Siagi, mafuta ya maji ya kupikia, sabuni za aina mbalimbali ikiwa ni pamoja na zile za kuoshea nywele (Shampoos).

Hali hii ni kashfa kubwa kwa taasisi hizi mbili kubwa nchini zilizopewa dhamana ya kuwalinda wananchi dhidi ya bidhaa zilizo chini ya ubora. Hii inaonyesha kwamba taasisi hizi zimeshindwa kutekeleza majukumu yake kikamilifu. Cha kusikitisha zaidi ni kwamba wizara husika zimeshindwa kuziwajibisha taasisi hizo.

Sikika inatoa wito kwa serikali pamoja na wizara husika kutekeleza mapendezo ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ikiwa ni pamoja na kubadilisa utawala wa uongozi wa Shirika la viwango Tanzania (TBS). Taarifa ya CAG iliyowasilishwa kwa kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali Kuu na Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma pamoja na kamati ya Bunge ya Viwanda na Biashara ilitaja thamani ya bidhaa hizo kuwa ni Tsh. 1.8 billioni ambazo zilikuwa chini ya kiwango na ziliweza kuingia sokoni. Bidhaa hizo zilikuwa zimekaguliwa na TBS na kuonekana hazifai kwa matumizi ya kawaida na matumizi ya binadamu.

Ripoti hiyo ya CAG inasema kuwa hata baada ya TBS kuamini kuwa bidhaa hizo zilikuwa chini ya kiwango, hakuna ushahidi wowote uliotolewa na taasisi hiyo kuwa bidhaa hizo zilirudishwa nchi zilikotolewa au kwamba ziliharibiwa. Hii inamaana kuwa bidhaa hizo zimeshaingia sokoni na kwa bahati mbaya zinaweza kuleta madhara makubwa kwa wananchi watakaozinunua na kuzitumia.

Ni kweli kwamba baadhi ya bidhaa hizo zina madhara ya moja kwa moja kwenye ngozi ya binadamu na kwa zile zinazotumika kama kinywaji zinaweza kuleta madhara makubwa ya kiafya kwa watumiaji walio wengi. Kwa bidhaa ambazo hazina kiwango kama vile vinywaji vya kuongeza nguvu, siagi na mafuta yatokanayo na mbegu za alizeti, kama yana sumu yanaweza kusababisha mtu kuugua sana na hivyo kusababisha mtu kupoteza maisha. Ni wazi kabisa kwamba athari kubwa itakayotokana na matumizi ya bidhaa hizi ni gharama za matibabu kitu ambacho ni sawa na kuongezea serikali mzigo kwenye kutoa huduma za afya ambazo hata kwa sasa hazitoshelezi.

Hii sio mara ya kwanza kwa TBS kuhusika katika kafsha kama hii. Mwaka 2011, kaimu mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma Bwana Deo Filikunjombe aliishutumu TBS kwa kuidanganya kamati hiyo kuwa wana ofisi nje ya nchi inayoshughulika na ukaguzi wa magari kabla ya kuingizwa nchini.

Sikika inaamini kwamba TBS na TFDA ni taasisi kubwa zenye uwezo mkubwa wa kudhibiti hali kama hii na hivyo kuhusishwa na taarifa kama hii ni sawa na kashfa ya kushindwa kazi. Pia, TBS na TFDA wanapaswa kutoa elimu endelevu kwa watumiaji jinsi ya kutambua bidhaa bandia na halali zikiwa sokoni kabla ya matumizi.

Sikika inashauri Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii pamoja na Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko kuchukua hatua za haraka ili kuzuia mzunguko wa bidhaa zilizotajwa. Pande zote zinazaohusika ambazo hazikutekeleza wajibu wao lazima ziwajibishwe na pale inapotakikana mkondo wa sheria utumike.


Bw. Irenei Kiria Mkurugenzi Mtendaji, Sikika, S.L.P 12183 Dar es Salaam,
Simu: +255 222 666355/57, Nukushi: 2668015, Barua-pepe: info@sikika.or.tz, Tovuti: www.sikika.or.tz

No comments: