TAARIFA YA KUKITHIRI KWA UHABA WA DAWA ZA MALARIA NCHINI
29
Januari 2013
1. UHABA WA ALu
Dawa muhimu za
malaria zijulikanazo kama dawa mseto (ALu) zimeripotiwa kuadimika katika vituo
vingi vya huduma za afya vya umma. Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kupitia mradi wa msonge (vertical
program) unaoratibiwa na Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Malaria (NMCP) wamekuwa
wakifuatilia uwepo wa dawa hizi kupitia nyenzo ya ufuatiliaji ijulinayo kama SMS for life ambayo imekuwa ikiwapa
picha kamili ya hali halisi ya dawa hizi katika vituo vyote vya huduma za afya
vya umma Tanzania bara. Ingawa nyenzo hii imekuwa ikitoa taarifa muhimu na kwa
wakati, kuna ushahidi mdogo kwamba taarifa hizi zimekuwa zikitumika kuhakikisha
vituo vya huduma za afya ambavyo vinapungukiwa ama kuishiwa ALu basi vinaletewa
kwa wakati. Sikika imekuwa ikifuatilia uwepo wa ALu kwa kutumia nyenzo hii kwa
takribani miaka miwili sasa na imegundua kutokuwepo kwa maendeleo yoyote. Tumeshuhudia
mara moja tu mwaka jana mwezi Mei, (2012) ambapo mamlaka husika zilichukua
hatua za dharura za kutatua tatizo la uhaba wa ALu katika vituo ambavyo
viliripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari kutokuwa kabisa na akiba ya ALu
ambapo asilimia 37 ya vituo vilivyokuwa
na uhaba kabisa ilishuka mpaka kufikia asilimia 24.
2. TAARIFA ZA HIVI
KARIBUNI ZA PROJECT YA SMS FOR LIFE
Kutokana na
taarifa za hivi karibuni (28/1/2013) kupitia project ya SMS for Life, vituo 1,300
(25.59%) kati ya vituo 5,080 katika mikoa 22 Tanzania Bara vimeripotiwa
kutokuwa kabisa na dawa mseto za aina zote (zero stocks). Uhaba huu umekuwa ukitofautiana baina ya mikoa na wilaya. Kwa mfano katika
mkoa wa Dodoma, ni asilimia 3 tu ya vituo vyote vya huduma ndivyo
vilivyoripotiwa kuwa na uhaba wa ALU, Singida (4%), Manyara ni (6%) na
Kilimanjaro (10%) wakati katika mkoa wa Mwanza, uhaba umeripotiwa kuwa ni
asilimia 57, Ruvuma (53%), Mara (46%), Kigoma (43%), Shinyanga (42%) na Tabora (41%).
Hali ni tofauti kabisa kwa wilaya hususani katika mikoa yenye uhaba mkubwa.
Mfano katika mkoa wa Mwanza, Wilaya ya Ukerewe imeripotiwa kuwa na uhaba wa ALu
kwa asilimia 88 katika vituo vyake vya huduma, ikifuatiwa na Sengerema (80%),
Geita (70%) na Misungwi (65). Hali hiii imekuwa ikijitokeza kwa kipindi kirefu
sasa ingawa kumekuwa na mipango na miongozo thabiti ya kupambana na Malaria.
Sikika ilifanya
utafiti (mwezi Machi, 2012 katika hospitali 54 Tanzania bara) na kubaini uhaba
mkubwa wa dawa za malaria ambapo asilimia 43 ya hospitali hizo hazikuwa na dawa
ya aina ya kwinini (kwa ajili ya kutibu malaria sugu) wakati asilimia 19 ya
hospitali zote hazikuwa na ALu.
3.
MAAMBUKIZI YA
MALARIA/VIFO VITOKANAVYO NA MALARIA
Malaria ni
ugonjwa hatari na unaoongoza kwa kusababisha vifo vya watanzania wengi,
hususani akinamama wajawazito na watoto
chini ya miaka mitano, hivyo upatikanaji wa dawa za malaria ni muhimu sana katika mapambano dhidi ya malaria pamoja na kupunguza vifo
hivyo.
Maambukizi ya
ugonjwa wa malaria kwa watoto chini ya miaka mitano Tanzania bara ni asilimia
18. Vituo vingi vya huduma vimekuwa vikiripoti kuwa malaria ndiyo inayoongoza
kwa kusababisha vifo kwa wagonjwa wa nje pamoja na wanaolazwa ambapo zaidi ya
asilimia 40 ya wagonjwa wa nje wanasumbuliwa na malaria. Hii inamaanisha kuwa
watu milioni 12-16 huugua malaria kwa mwaka. NMCP inakadiria vifo vitokanavyo
na malaria Tanzania kufikia 60,000 – 80,000 kwa watu wa rika zote. (Extrapolated from the under-five mortality
rate in 2004-05 TDHS, size of under-five population, and the proportion of
deaths attributable to malaria).
Kutokana na takwimu za Tanzania HIV & Malaria indicator survey 2007/2008, maambukizi
ya malaria baina ya mikoa, Mwanza inaonekana kuwa na maambukizi ya malaria kwa
asilimia 31 ikifuatiwa na Ruvuma (24%),
Mara (30%), Kigoma (20%) na Shinyanga (30%) wakati mikoa hii ndio inayoongoza
kwa kuwa na uhaba mkubwa wa dawa za malaria.
4. FEDHA KWA AJILI YA KUZUIA NA KUTIBU MALARIA
Miradi ya
kupambana na Malaria imekuwa ikifadhiliwa na wafadhili mbalimbali, hususani Global
Fund, Mfuko wa ufadhili wa Raisi wa Marekani (PMI – USAID), Benki ya dunia
(World Bank) pamoja na wahisani wengine. Global Fund ndiyo inatoa ufadhili
mkubwa kwa asilimia 57, PMI – USAID (33%), World Bank (6%) na vyanzo vingine
(4%) . Tangu 2003 mpaka 2010 malaria ilifadhiliwa kwa takribani dola za
kimarekani milioni 450., Serikali kupitia NMCP ndiyo imekuwa ikiomba fedha hizi
kupitia Global Fund kwa ajili ya ununuzi wa dawa za malaria, hivyo kama
kunakuwa na ucheleweshwaji wa fedha kutoka Global Fund, serikali ina uwezo wa
kutafuta fedha kutoka PMI ili kusaidia kupunguza uhaba wa dawa hizi. Hivyo ni
jambo la kusikitisha kuona kwamba vituo vingi vya huduma vinakuwa na uhaba wa
ALu.
5. MAHITAJI YA DAWA ZA ALU UKILINGANISHA NA KIWANGO
KINACHOAGIZWA
Kwa wastani,
matumizi ya dawa za ALu nchini Tanzania ni dozi million 1.3 kwa mwezi. Hii inamaanisha
kwamba ni karibu dozi 15,600,000 kwa mwaka. Hata hivyo
tukiangalia katika taarifa zinazopatikana kwenye ripoti ya Global Fund (kupitia ripoti za AMF)
tunaona kwamba kwa kipindi cha 01 Januari 2012 mpaka 17 Januari 2013 Tanzania
iliagiza na kupokea dozi 4,917,780 kwa sekta ya umma kupitia Bohari Kuu ya Madawa
(MSD) kwa awamu nne kwa mwaka. Wakati tunaona sekta ya binafsi iliweza kuagiza
na kupokea dozi 11,527,990.
6.
MAPENDEKEZO
Mpango wa Taifa
wa Kudhibiti Malaria (NMCP) uliopo chini ya wWizara ya Afya na Usatwi wa Jamii (MOHSW)
ndio unaowajibika kusimamia shughuli zote zinazohusiana na kupambana na Malaria
nchini. Mpango huu unasimamia ufadhili,
kutathmini mahitaji na kupanga ratiba za ununuzi na usambazaji. Na hivyo
basi inawajibika kwa hali inayoonekana sasa ya dawa hii muhimu ya ALu katika
sekta ya umma. Sikika imeona kwamba NMCP haijaonyesha juhudi zinazostahili katika kukabiliana na upatikanaji wa dawa za
ALu.
Ili kumaliza uhaba
huo sugu na kuishiwa dawa mara kwa mara, Sikika inashauri kwamba MOHSW na NMCP watafute
rasilimali fedha za kutosha ili waweze kununua dawa za Alu kwa kiwango kikubwa,
ikibidi za mwaka mzima kwa mkupuo mmoja (dozi milioni 15.6), na kisha
kuhakikisha kwamba kuna dawa za ziada za
kutosha angalau kila baada ya miezi 6. Kushindwa kutekeleza hayo
kutasababisha uhaba huo kuendelea, hali ambayo itaongeza idadi ya wagonjwa
pamoja na vifo vinavyotokana na malaria.
Mr. Irenei Kiria, Executive
Director of Sikika, P.O.Box 12183 Dar es Salaam,
Tel: +255 222 666355/57, Cell:
0784 274039, Fax: 2668015, Email:info@sikika.or.tz,
Twitter: @sikika1, Facebook: Sikika Tanzania, Website: www.sikika.or.tz
[1] Mahitaji halisi yanaweza kuzidi kuzidi idadi iliyotajwa, wataalamu wengine
wamekadiria mahitaji halisi kuwa kati ya milioni 18 hadi 25.
No comments:
Post a Comment