TAMKO
KUHUSU UHABA WA DAWA MSETO ZA KUTIBU MALARIA (ALU) –FEBRUARI 10, 2012
Sikika
imeshangazwa na taarifa za Wizara ya Afya na Ustawi waJamii kwamba kuna dawa za
kutosha aina ya ALU za kutibu malaria hapa nchini wakati ambapo vituo vya kutolea
huduma vya umma vina uhaba mkubwa wa dawa aina hiyo.
Taarifa
hiyo iliyotolewa na Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo tarehe 1/2/2013, na
kuchapishwa kwenye baadhi ya vyombo vya habari ilikuwa ikikanusha tamko
lilitolewa na Sikika kwenye vyombo vya habari kuhusu uhaba wa dawa mseto (ALu) kwenye
vituo 1300 (26%) vya umma vya huduma za afya nchini.
Sikika inaikumbusha Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii
kwamba kuna tofauti kubwa kati ya shehena zinazoagizwa nchini, na uwepo wa dawa
hospitalini. Taarifa iliyotolewa na Sikika ilisisitiza kutokuwepo kwa dawa katika
vituo vya kutolea huduma wakati taarifa ya wizara ilihusu shehena za dawa zilizoingia
nchini na zinazotarajiwa kuingia.
Pamoja
na Wizara kutumia nguvu na muda mwingi kukanusha uhalisia wa taarifa za uhaba
wa dawa za ALu nchini, hali halisi bado
inaonyesha kuwepo ukosefu wa dawa hizo kwenye baadhi ya vituo hadi leo tarehe
10 Februari, 2013. Taarifa ambazo zinapatikana kutoka katika mtandao wa Wizara ya
Afya na Ustawi wa Jamii kupitia mfumo wa kielektroniki ujulikanao kama ‘SMS for life’, zinaoonesha kwamba hadi
kufikia leo, asilimia 25 (vituo
1,280) ya vituo vya afya vya umma nchini
bado havina dawa zozote aina ya ALu.
Mfumo
huo pia ulionesha kwamba mikoa iliyoripotiwa na Sikika kuwa na ukosefu wa dawa
(ALU na Quinine) uliokithiri hapo Januari 28, 2013 bado ilikuwa haijafikishiwa
dawa zinazodaiwa kuwepo nchini. Mikoa hiyo na asilimia ya idadi ya vituo
ambavyo havina dawa hizo (ALU na Quinine) katika mabano ni; Mwanza(59%), Ruvuma
(49%), Shinyanga (44%), Tabora (40%), Mara (38%), na Kigoma (38%).
Kwa
hali hiyo, Sikika ingependa kuamini kuwa taarifa ya Wizara kwamba dawa za ALU zipo
nchini ni za kweli. Lakini, kama taarifa hizo ni za ukweli, kwa nini hizo dawa hazipo kwenye vituo vya
kutolea huduma kwa takribani asilimia 25 kwa miezi kadhaa sasa? Je, Wizara
inataka kueleza wananchi kwamba mfumo
wake wa kielektoniki (SMS for life) hautoi takwimu za ukweli?
Taarifa
ya Wizara ilidai pia kwamba mfumo wake
huo wa kielektoniki (SMS for life), unahusika na dawa za kutibu malaria aina mbili tu
ambazo ni Alu na Quinine na sio dawa nyingine za kutibu Malaria. Katika hilo, Sikika inapenda kukumbusha umma kwamba tangu mwaka 2006,
Tanzania imekuwa ikifuata mwongozo wa matibabu ya malaria uliotolewa na Shirika
la Afya Duniani (WHO), unaotumia dawa ya
ALu kutibu malaria ya kawaida na Quinine
kwa malaria sugu huku SP ikitumika kwa akinamama wajawazito.
Kwa
mantiki hii, Sikika inaiomba Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kutaja hizo dawa aina zingine zinazotumika
kutibu malaria ya kawaida, ambazo hazipo
katika mfumo wa ‘SMS for life’. Pia
Wizara hiyo ieleze umma dawa hizo nyingine ambazo haijazitaja zinatumika kwa
kufuata mwongozo upi na ulipitishwa na taasisi gani? Je, ni lini watoa huduma walipata mafunzo ya
namna ya kutumia hizo dawa aina nyingine?
Badala
ya kuendeleza malumbano, Sikika inatoa rai kwa
Wizara ya Afya kuutumia vyema mfumo wake wa SMS for life kwa kujipanga ili kuhakikisha afya za watanzania
zinalindwa na kwamba uhaba wa mara kwa mara wa dawa za Alu pamoja na zingine
kwenye vituo vya huduma za afya, hautokei tena.
Mr. Irenei Kiria
Executive Director of Sikika, P.O.Box 12183 Dar es Salaam,
Tel: +255 222 666355/57, Fax: 2668015, Email: info@sikika.or.tz,
Website: www.sikika.or.tz
No comments:
Post a Comment