TAMKO LA ASASI ZA KIRAIA
|
MKUTANO WA WADAU WA KUTATHMINI SEKTA YA AFYA
Waheshimiwa
Mawaziri, Katibu Mkuu,
Wabunge, Mganga Mkuu, Washirika wa Maendeleo Wafanyakazi wa Wizara ya Afya,
TAMISEMI, Utumishi, wawakilishi wa sekta binafsi, mabibi na mabwana, habari za
asubuhi!
Tunatoa shukrani zetu za dhati kwa kupata
nafasi hii kuwa watu wa mwanzo kuzungumza katika siku hii ya Sera kwa wadau wa
sekta ya afya hapa Tanzania.
Sikika inasoma taarifa hii kama mwanachama
hai wa Policy Forum. Policy Forum ni jumuiko la asasi za kiraia lenye wanachama
wapatao 100 ambao wanalenga kuhimiza ushirikishaji wa taasisi za kiraia katika
maamuzi na utekelezaji wa sera zinazomhusu mwananchi wa kawaida wa Tanzania.
Mheshimiwa
Waziri, tunapenda kuanza
kwa kuipongeza Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii (MoHSW) kwa kufanya tathmini
ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Afya III (HSSP). Tumeridhika kuona kwamba taarifa
ya utekelezaji wa mpango mkakati huo imeleta matokeo na mapendekezo ambayo tukiyafanyia
kazi kwa pamoja, tunaweza kuboresha utendaji wa sekta ya afya hapa nchini.
Tunapenda pia kupongeza sekta ya afya kwa
mafanikio mengi yaliyopatikana kwa mwaka uliopita kama vile muendelezo
unaofanywa wa kuimarisha mfumo wa rasilimali fedha na pia uimarishaji wa Bohari
ya Dawa ya Taifa (MSD) ambao umeiwezesha kutunukiwa cheti kutoka Shirika la Kimataifa la Viwango duniani kwa
kuimarisha na kudhibiti ubora.
Mheshimiwa
Waziri, licha ya juhudi
zinazofanywa, bado bajeti inayotengwa kwa ajili ya sekta ya afya ni ndogo na
haitoshelezi mahitaji yaliyowekwa kwenye mpango mkakati wa sekta ya afya. Bajeti
ya sekta ya afya bado inategemea mno wahisani, hivyo kutishia maendeleo
endelevu ya mfumo mzima wa afya.
Mabibi
na mabwana, ilikuwa ni
miongo miwili iliyopita, mwaka 1993, wakati serikali ilipoanzisha sera ya
uchangiaji ili kuongeza rasilimali na kukuza ushirikishaji wa wananchi. Hata
hivyo, watoa huduma za afya wameripoti kwetu vikwazo na changamoto
wanazokumbana nazo katika kuwatambua watu wanaostahili kupata huduma za afya
bure. Kwamba, nani anahusika kulipa au kufidia gharama za wanaostahili kupata
matibabu bure, bado ni swali ambalo halijajibiwa.
Kuonyesha ukubwa wa hili tatizo, mathalan,
asilimia 75 ya wagonjwa wote katika hospitali ya Mwananyamala wako katika
daraja la watu maskini, na hivyo kustahili msamaha wa matibabu. Takwimu
zilizopatikana kutoka hospitali ya Temeke zinaonyesha gharama za kutoa huduma
kwa watu wenye msamaha wa gharama za matibabu zinakua mwaka hadi mwaka. Kwa
mwaka wa fedha 2010/11 zilitumika dola 661,000/-, kwa 2011/12 zilitumia dola
710,000/-, na 2012/13 hospitali ilitumia kiasi cha dola 1,504,000/-. Ukilinganisha
gharama hizi na uwiano wa mapato yaliyokusanywa katika miaka hiyo, ni sawa na
kiasi cha dola 375,000/- kutoka kwa kila mgonjwa ambaye anaweza kulipia.
Mheshimiwa Waziri, AZAKI zinaishauri Serikali kuchukua hatua kwa
kukuza na kubuni mikakati ya fedha
ambayo itajikita kuelekeza vyanzo vipya vya rasilimali kwenye sekta ya
Afya. Hili linaweza kufanyika kwa kupanua
wigo wa mifumo ya mfuko wa bima ya afya ya jamii, kupunguza matumizi yasiyo ya
lazima na kutekeleza shughuli madhubuti zitakazoleta matokeo ya kimkakati. Zaidi,
tunashauri kupitia upya mwongozo wa uchangiaji gharama ili kupunguza mzigo wa
madeni kwenye gharama za uendeshaji.
Mheshimiwa Waziri, Sikika kwa kushirikiana na Chama cha Madaktari
Tanzania (MAT), ilifanya utafiti ambao ulilenga katika kuangalia walipo na
wanapokwenda wahitimu wa fani ya udaktari Tanzania. Matokeo ya utafiti huo yalionesha
kuwa asilimia 40% ya madaktari wahitimu hawaendelei na fani ya udaktari. Na
takribani 42% ya wahitimu wa fani ya udaktari wamebaki katika miji mikubwa, kwa
mfano, Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Mbeya na Kilimanjaro. Na 32% ya madaktari
wote waliohusishwa katika utafiti huu walikuwa katika Jiji la Dar es Salaam.
Kutokana na matokeo ya utafiti
huu, AZAKI zinashauri mamlaka husika kuboresha mazingira yatakayowavutia
madaktari na kuwafanya waendelee kuwepo na kufanya kazi katika fani yao, hasa
katika maeneo ya vijijini ambayo watanzania walio wengi wanaishi.
Mheshimiwa Waziri, AZAKI zimeshuhudia changamoto nyingi za
upatikanaji na uwepo wa madawa muhimu na vifaa tiba nchi nzima. Hali hii
inatokana na mambo mengi kama vile upungufu wa bajeti na changamoto katika
mfumo wa ugavi na usambazaji wa dawa. Kwa mfano, makadirio ya fedha zote
zilizohitajika kwa ununuzi wa madawa katika mwaka wa fedha 2012/12 ulikuwa Tsh.
198 bilioni, wakati huo fedha zilizopatikana ni Tsh. 80 bilioni, sawa na 40%. Utafiti uliofanywa na Sikika 2012 katika
kuangalia uwepo na upatikanaji wa madawa na vifaa tiba muhimu katika hospitali
za Serikali ulionesha kwamba 96% ya madawa yaliyotakiwa kuwepo hayakuwepo
katika hospitali na 94% ya hospitali hizo hazikuwa na ama aina moja ya dawa na
vifaa tiba muhimu au vyote.
Ili kuweza kukabiliana na mgawanyo
huu usio sawia, ni vyema fedha zote zinazotolewa kwa ajili ya madawa na vifaa
tiba zipelekwe katika vituo vya kutolea huduma kwa kuzingatia mfumo wa
kukokotoa mgawanyo. Hadi sasa, bado mfumo huo wa ukokotoaji wa mgawanyo wa dawa
kulingana na mahitaji unakabiliwa na
changamoto nyingi ingawa juhudi zinafanyika kuboresha taarifa na kuanza
utekelezaji.
Mheshimiwa Waziri, tunaipongeza Wizara yako kwa kulifanyia kazi
suala la ARV bandia zilizosambazwa katika vituo vya kutolea huduma za afya mwanzoni
mwa mwaka huu. Hata hivyo, upelelezi wa polisi katika suala hili umechukua muda
mrefu sana na haieleweki ni lini watuhumiwa watawajibishwa.
Mheshimiwa Waziri, wakati sekta ya afya
inajikongoja katika utoaji wa mashine za kupima VVU (CD4), Shirika la Afya Duniani
limependekeza utoaji wa dawa za kupunguza makali ya VVU kutolewa mapema,
angalau kwa wenye CD4 500 (500 CD4 cells/mm3)
badala ya kipimo cha sasa cha CD4 350 (350CD4
cells/mm3). Hii inamaanisha kwamba, watu wengi zaidi watahitaji kupima VVU
na kuanza kutumia ARVs. Tunatarajia mabadiliko haya yatazingatiwa katika mipango na makadirio ya fedha kwenye
bajeti ijayo.
Mabibi na mabwana, ripoti ya ukaguzi wa fedha wa Wizara ya Afya ya mwaka 2011/12 iliibua matatizo
mbalimbali ikiwemo utunzaji mbaya wa kumbukumbu, usimamizi duni wa bajeti na
mali za Wizara. Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu ya Serikali (CAG) ana mamlaka
kikatiba kutoa mapendekezo kwa Mhasibu wa Wizara ambaye anawajibika kulinda fedha
na mali za umma. Ndio maana tunasikitika kuona kwamba, hata baada ya mwaka
mmoja kupita, hoja 13 zilizoibuliwa na CAG zinazofikia kiasi cha Tsh. 71
bilioni, bado hazijafanyiwa kazi. Kufuata na kuzingatia sheria na kanuni za
fedha ni muhimu ili kudumisha imani kwa wananchi katika usimamizi wa huduma za
afya ya jamii.
Mheshimiwa Waziri, Asasi zinapendekeza kuwa hoja zilizoibuliwa
wakati wa ukaguzi wa mahesabu zishughulikiwe
na kutatuliwa kwa haraka.
Tunaipongeza serikali ya Tanzania
kwa kujiunga na Ushirikiano wa Uwazi wa Serikali (OGP) na ahadi ilizoweka katika mpango wa
utekelezaji wa 2012-2013 ili kukuza
uwazi. Pamoja na nia hiyo nzuri ,tovuti ya Wizara ya Afya bado haina taarifa
nyingi muhimu hasa katika eneo la ununuzi na utaratibu wa usambazaji. Utafiti
wa hivi karibuni uliofanywa na Sikika umegundua kwamba asilimia 36 ya
wazabuni wa ugavi wa aina mbalimbali za
dawa kwa MSD wamelalamikia kukosekana kwa uwazi katika mchakato wa zabuni.
Tunapendekeza kwamba Wizara ya
Afya na Ustawi wa Jamii ianze kuweka
taarifa mbalimbali za umma kwenye tovuti yake na maeneo mengine ya wazi ambapo
walipa kodi na wadau wengine muhimu wanaweza kuzifikia kwa urahisi.
Mheshimiwa Waziri, uwazi katika mgawanyo wa fedha kwenye wizara
bado ni suala nyeti. Katika mwaka huu wa fedha, Wizara imepanga kutumia kiasi
cha shilingi 283 bilioni kwa ajili ya matumizi ya kawaida. Takriban theluthi
mbili ya kiasi hiki cha fedha kitagawanywa kwa
taasisi na Idara nje ya Wizara kwa
njia ya misaada, ruzuku, michango na mifumo mingine ya misaada. Hata hivyo,
hakuna ufafanuzi wa jinsi fedha hizo zitakavyotumika.
Asasi zinapendekeza kuwa umma upewe taarifa za
ziada zinazochanganua jinsi idara na taasisi hizo zitakavyotumia fedha za
walipa kodi.
Mheshimiwa Waziri, mwisho tunapendekeza ushirikishaji wa wananchi
katika mipango ya afya, ufuatiliaji na usimamizi kwa kuwa kufanya hivyo ni
muhimu katika kuelekea uboreshaji wa utoaji huduma za afya. Tumeshuhudia
mafanikio kupitia mbinu ya ufuatiliaji wa uwajibikaji jamii ambayo inahusisha
wananchi katika ufuatiliaji wa mipango ya huduma za afya, fedha na utoaji
huduma katika ngazi ya wilaya. Asasi zinashauri serikali iwekeze katika mbinu
za ushirikishaji jamii ili kuboresha utolewaji wa huduma za afya katika ngazi za
Wilaya.
Mheshimiwa Waziri, Mabibi na Mabwana, tunawashukuru tena kwa nafasi
hii ya kuhutubia washiriki kwenye siku hii ya Sera na tunategemea ushirikiano wetu utaendelea
kuzaa matunda kwani sote tuna mchango muhimu katika kuboresha sekta ya afya.
Asanteni!
Imewasilishwa na Bw. Irenei Kiria,
Mkurugenzi Mkuu wa Sikika, kwa niaba ya Policy Forum
No comments:
Post a Comment