UTANGULIZI
Sheria hii ya makosa ya
mtandao, 2015 imebainika kuwa na mapungufu makubwa sana. Mapungufu hayo
yamebainika kuwa, kama sheria ikipita yanaweza kuifanya nchi ikawa ni kati nchi
adui za matumizi ya mtandao wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano duniani.
Watanzania wote wanatakiwa
kufahamu kuwa muswada ukipita utatumika nchini kote yani Tanzania Bara na Visiwani.
Watanzania walio wengi
hawafahamu Sheria hii inawahusu kwa namna gani; lakini kwa lugha rahisi ni kuwa
itamuathiri mtu yeyote anayeweza tumia mtandao wa intaneti kwa kutimia kifaa
chochote iwe kompyuta kubwa au vifaa vyenye uwezo wa kufanya kazi kama kompyuta
kama Simu za mikononi, saa, televisheni na vifaa vingine vinavyoendana na
hivyo.
Malengo ya Sheria hii ni
kuainisha makosa yanayohusiana na matumizi ya mfumo wa kompyuta na Teknolojia
ya Habari na Mawasiliano, kuweka utaratibu wa upelelezi, ukusanyaji na matumizi
ya ushahidi wa kielektroniki na masuala mengine yanayohusiana na hayo.
Matumizi ya mitandao yote
mikubwa kama Twitter, Instagram, JamiiForums, Facebook, Barua pepe, WhatsApp,
blogu na data zote zilizo katika kifaa chochote cha kielektroniki yanaathiriwa
kwa kiwango kikubwa na Muswada huu.
UCHAMBUZI
Ibara ya 4
Ni computer gani inazungumziwa
hapa? Ya nani?
Ibara ya 5
Computer gani inayokusudiwa,
ya nani?
Ibara ya 7
(1-3):
Haibainisha ni aina gani za data ambazo haziruhusiwi kuguswa/kufutwa au
zikiguswa/futwa ni kosa la jinai.
7(1g): Kipengele
hiki katika ibara hii kinarudiwa mara kadhaa katika (Ibara za 32-35). Badala ya ibara za mbele kurejea ibara hii,
watunga sheria wameiacha ibara hii ikiwa haieleweki hadi mtu asome ibara za
mbele.
Je mtu aliyeidhinishwa katika
ibara na kipengele hiki ni nani?
Ibara ya 8:
Muswada huu haujaweka bayana iwapo
nyaraka za siri zinaweza kuwekwa
wazi katika mtandao kama zina maslahi ya nchi au wananchi mf. Matumizi mabovu
ya pesa za umma
Ibara ya 14:
Neno pornografia halijapewa
maana na hivyo jambo lolote lenye mwonekano wa kiasherati (sexually vulgar) linaweza
kutafsiriwa kama pornografia na kumuingiza muhusika matatizoni.
Ponografia ya mtandao
isikatazwe kabisa ila inatakiwa kuweka
ulinzi thabiti wa kuhakikisha watoto hawawezi kufungua mitandao ya aina hiyo.
Ponografia zote ni chafu
lakini sio chafu zote ni ponorafia. Hivyo kutokana na kuwa sheria hii inasema
ponografia zote ni chafu hii
itasababisha kila mtu ahukumiwe chini ya kifungu B.
Uchafu na Ponografia viwe
vipengele viwili tofauti.
Artcile 15:
Suala la kujifanya mtu
mwingine kwenye mtandao, linaweza kuleta utata kwani kuna baadhi ya mitandao
ambapo watumiaji hutumia majina ambayo sio ya kwao. Itakuwaje watu kwa
madhumuni mabaya wakitafuta mtu mwenye jina kama hilo na kumshtaki mtumiaji
wa mtandao?
Je, mtu kujifanya mtu
mwingine inahusisha mtu kutumia jina lisilo lake hata kama hajajifanya mtu
mwingine? Ni vema suala hili likafafanuliwa kisheria kwakuwa ni suala muhimu
lakini wachache wataelewa manaa yake.
Ibara ya 16:
Ni nani ana mamlaka ya
kubainisha kuwa jambo lililowekwa kwenye mtandao ni la UKWELI, UONGO au UPOTOSHAJI?
Ni wazi kuwa mamlaka husika inaweza tumia hili kama mtego kwa manufaa yao.
Kipengele hiki kama vingine
kimeambatanisha muda usiopungua bila kusema muda usiozidi. Hivyo mtuhumiwa
anaweza kufungwa hata kifungo cha maisha kutokana na mamlaka ya mahakama.
Watu binafsi wanaweza kutumia
vibaya kifungu hiki kuzuia uhuru wa maoni kwa kuwaburuza watumiaji wa mtandao
mahakamani kila kukicha na kuwapotezea muda wahusika ambao wanaweza kubainika
mwishoni kuwa walionewa.
Ibara ya 20:
Katika mawasililano ya
mtandao kama ilivyo mawasiliano mengine kuna ujumbe ambao mtu hawezi kuacha
kuupata
Mfano kutembea barabarani na kuona bango la matangazo,
au kuwa ndani ya daladala iliyowasha redio.
Vivyo hivyo katika mtandao sio kila ujumbe anaopokea
mpokeaji ameuomba na hivyo kifungu hiki kinafanya kila mtu atakayepokea ujumbe
bila ridhaa yake kuwa amefanya kosa la jinai.
Ibara ya 21(1):
Tafsiri za Kiswahili na
kiingereza zipo tofauti kabisa.
Ya Kiswahili inamlenga mtoa
huduma na huku ya kingereza inamlenga mtu
yeyote anayetumia mtandao.
Ya Kiswahili inamlazimu mtoa
huduma kumtaja mhusika aliyeweka ujumbe na pia kumuadhibu mtoa huduma huku ya
kiingereza inazungumzia kuhusu tafiti kwa ujumla.
Ya kiingereza ni nzuri lakini
ya Kiswahili imepotoshwa kabisa na inavunja uhuru wa mawasiliano.
MUHIMU:
Hakuna kinga yoyote kwa mtoa
taarifa (source) kwa mujibu wa ibara hii.
Ibara ya 22:
Je, nani ana mamlaka ya
kuamua kuwa ujumbe kwenye mtandao unatolewa au kuboreshwa kwa kusudi au bila
kusudi.
Itambulike kuwa ujumbe wa
kwenye mtandao huboreshwa (edit) au kufutwa wakati wowote muhusika anapoona
inafaa mf. Whatsap status, fb status etc.
Ibara ya 23:
Unyayasaji wa kupitia mtandao
(cyber bullying) haujapewa maana.
Sheria inatakiwa kuweka
bayana maudhi ya kihisia ni nini.
Kwani mtu yeyote atakayeudhiwa
‘kihisia’ au kudai kuwa hisia zake
zimeudhiwa anaweza kushtaki. Sio kila linalosababisha maudhi ya kihisia ni
unyanyasaji
Ibara ya 27:
Ni nani anaamua kitendo fulani
ni kula njama? Mazungumzo ya kawaida na maamuzi ya kukubalika na upande
mmoja yanaweza kutafsiriwa kama kula njama na watu wa upande mwingine.
Ibara ya 31 (3a):
Sheria ya kiingereza inasema
‘as soon as practicable’ lakini ya
Kiswahili inasema wakati wa upekuzi na ukamataji wa mali. Hizi zina maana
tofauti.
Ibara hii inawapa mamlaka
Wakuu wa Vituo vya Polisi kufanya upekuzi na kuchukua mali(za kielektroniki) na
taarifa binafsi za raia bila amri ya Mahakama.
Ibara ya 32-35
Ibara hizi zinamlazimisha
mtoa huduma kutoa data za wateja wake kwa Mkuu wa kituo cha Polisi bila kibali
cha Mahakama. Wakuu wa Vituo vya Polisi wamepewa nguvu sana katika sheria hii!
Mahakama ipewe mamlaka haya na si Polisi, na ifanyike hivi baada ya
kujiridhisha kuwa mwananchi anatakiwa kufanyiwa upekuzi, kuchukuliwa data zake
au za wateja wake n.k
Ibara ya 39-45
Watoa huduma na wahifaji
tovuti wanalindwa na ibara hizi lakini kwa masharti.
Katika ibara ya 39, Waziri
anapewa mamlaka ya kuamua kipi ni kosa na kipi si kosa. Anapewa mamlaka ya
kusimamisha na kusitisha huduma, kuondoa taarifa juu ya kitendo husika (mfano
kulazimisha kuondoa mijadala yote ya ufisadi flani kama yeye ataona kwa mamlaka
yake kuwa haufai kujadiliwa).
Muswada huu ibara za 31-38 na
ibara za 39-46 zinakinzana kwani kwa wakati mmoja mtoa huduma anaweza akawa
ameona jambo ameshalitoa na anajiandaa kuitaarifu mamlaka husika huku mamlaka
husika (Askari Polisi) ikiwa na uwezo wa kwenda kuchukua vifaa na data za mtoa
huduma.
Mamlaka ya Polisi imepewa
kinga kubwa ambayo haiingiliani na sheria yoyote ile.
No comments:
Post a Comment