Pongezi Serikali kwa Hatua Kuimarisha Upatikanaji Dawa
... iboreshe
mifumo kuongeza upatikanaji
Mara kwa mara, tumekuwa
tukitoa matamko na mapendekezo ili kuboresha upatikanaji wa huduma za afya kwa
wananchi, hususan dawa na vifaa tiba. Kwa
ujumla, hali ya upatikanaji wa dawa nchini inaanza kuimarika ingawa bado kuna baadhi
ya changamoto ambazo tuna imani zinaweza kushughulikiwa.
Ufuatiliaji wa
Sikika uliofanyika kupitia mahojiano na wananchi waliotoka kupata huduma za
afya, asilimia 81 ya waliohojiwa mwaka
2017 waliweza kupata dawa zote walizoandikiwa ukilinginisha na asilimia 51 ya
wananchi waliohojiwa mwaka 2016 (ongezeko la asilimia 30). Ufuatiliaji huu
ulifanyika katika wilaya ambazo Sikika inafanya kazi. Sikika inaipongeza
serikali kwa hatua inazochukua katika kuimarisha upatikanaji wa dawa nchini hasa
ikikumbukwa kwamba:
Kwanza, kulikuwepo
malalamiko juu ya gharama za baadhi ya dawa zinazosambazwa na Bohari Kuu ya
Dawa nchini, (MSD) kulinganisha na za wauzaji binafsi. Suala hili limefanyiwa
kazi kwa kiasi kikubwa kwa kuanzisha utaratibu wa kuagiza dawa moja kwa moja
kutoka kwa wazalishaji, viwandani. Kwa mujibu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
(MOHCDGEC), utaratibu huu umepunguza gharama za
dawa kwa kati ya asilimia 15 hadi 80, hivyo kuongeza upatikanaji wa dawa
vituoni, kwa gharama nafuu.
Pili, kwa miaka
miwili mfululizo kumekuwa na ongezeko la bajeti ya dawa ambayo ni hatua nzuri
kwa serikali katika kuboresha huduma za afya. Fedha zilizokuwa zimetengwa kwa
ajili ya dawa kwa mwaka wa fedha 2016/17, (Tsh bilioni 251) zilitolewa kwa
kiasi kikubwa (Tsh bilioni 132) ikilinganishwa na mwaka wa fedha 2015/16 ambapo
zilitengwa Tsh bilioni 31 na kutolewa Tsh bilioni 24. Hatua hii imeiongezea MSD
uwezo wa kuagiza na kununua dawa, na hivyo kuongeza upatikanaji wake vituoni.
Tatu, kwa miaka
kadhaa Sikika imekuwa ikiishauri
serikali iondoe ukiritimba wa MSD kuwa sehemu pekee ambapo vituo vinatakiwa kununua
dawa. Hii imekuwa ikisababisha matatizo pale ambapo dawa husika hazipatikani
MSD na vituo haviruhusiwi kununua sehemu nyingine hata kama vina fedha. Kwa
sasa, vituo vya huduma vimeruhusiwa kununua dawa kutoka kwa wauzaji binafsi pindi
zinapokosekana MSD.
Tumefurahishwa na mipango
ya maboresho na mgawanyo wa majukumu kati ya MOHCDGEC na TAMISEMI katika kusimamia utoaji
wa huduma za afya ikiwemo upatikanaji wa
dawa vituoni. Utawala wa vituo vya afya na idara za afya katika halmashauri
umeimarika zaidi.
Pamoja na pongezi
hizi, kuna changamoto kadhaa ambazo tungependa kuona serikali ikiendelea kuzifanyia
kazi.
· Kwanza, MSD iimarishe mawasiliano na wadau,
hususan kwa kutoa taarifa muhimu ili kuimarisha ufuatiliaji na uwajibikaji
katika mfumo wa ugavi. Mfano, kutoa taarifa za upatikanaji wa dawa kupitia
tovuti yao kama ilivyokuwa awali.
· Pili, MSD kuwa mnunuzi na msambazaji pekee
wa dawa bado ni changamoto kwasababu nchi ni kubwa kijiografia na vituo vya
huduma ni vingi (zaidi ya 5000). Hivyo basi tunapendekeza kwamba MSD isiwe
mshitiri pekee. Kwa Mfano, ongezeko la sasa la upatikanaji wa dawa vituoni
haukutokana na MSD pekee bali pia uwezo wa vituo kukusanya fedha na kununua
dawa kutoka kwa wauzaji binafsi.
· Tatu, kumekuwa na changamoto kwenye
upatikanaji wa vifaa na vifaatiba katika
vituo vingi vya huduma vya afya na hivyo wagonjwa kupewa rufaa zisizo za
lazima. Serikali iwekeze katika kununua vifaa hivyo na kukarabati vilivyopo ili
kuongeza ubora wa huduma.
· Nne, kumekuwa na malalamiko kwamba baadhi
ya dawa katika baadhi ya vituo zinapotea. Serikali iweke mifumo imara ya kudhibiti upotevu wa dawa vituoni. Mfumo ulioanzishwa wa
kielektroniki wa kuendesha hospitali (GoT-HoMIS) ukisimikwa vituo vyote nchini
utaweza kusaidia kupunguza tatizo hili.
Irenei Kiria
Mkurugenzi Mtendaji- Sikika, SLP
12183 Dar es Salaam,
Twitter: @sikika1,
Facebook: Sikika Tanzania, Instagram: sikikatanzania
No comments:
Post a Comment