18 Februari, 2013
Sikika inapenda kumpongeza Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii,
Dk. Hussein Mwinyi kwa kuweka bayana na kukiri kwamba kuna uhaba mkubwa wa dawa
muhimu za kutibu malaria, maarufu kama dawa mseto (Alu) katika vituo vingi vya
huduma za afya vya umma nchini.
Akizungumza
na vyombo vya habari hivi karibuni, waziri Mwinyi alikiri kuwepo kwa uhaba wa
dawa hizo za kutibu malaria kama zilivyoripotiwa na mtandao wa Wizara hiyo
kupitia mfumo wa kielektroniki ujulikanao kama ‘SMS for Life.’ Dk. Mwinyi alinukuliwa akiwataka watanzania kutokuwa na wasiwasi
kwani suala hilo lilikuwa linashughulikiwa na kwamba usambazaji wa Alu
ulishaanza.
Taarifa
ya Kikuli pia ilikaririwa na vyombo vya habari ikiueleza umma kwamba kuna dawa nyingine za malaria
ambazo haziripotiwi kupitia SMS for life,
jambo ambalo si kweli.
Sikika
inaiomba Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kuharakisha usambazaji wa dawa hizi
na ilichukulie suala hili kama dharura kwani kuna baadhi ya vituo vya huduma
vina uhaba mkubwa wa Alu kwa takribani siku 300 sasa. Pia tunaishauri Wizara
kubadili mfumo wa uagizaji wa dawa kwa zahanati na vituo vya afya ambao huvilazimu vituo kuagiza dawa kila
baada ya miezi mitatu (robo mwaka), wakati usambazaji wake unachukua muda wa
miezi miwili hadi mitatu. Ni vyema vituo viwe vinaagiza dawa kila mwezi ili
kupunguza tatizo la uhaba wa dawa muhimu unaojitokeza mara kwa mara.
Ikumbukwe
kwamba msimu wa mvua unakaribia kuanza katika maeneo mengi hapa nchini na hivyo
kuwepo kwa uwezekano wa kuongezeka kwa maambukizi ya malaria. Ugonjwa wa
malaria unaongoza kwa kusababisha vifo vingi nchini. Hivyo basi,
uwepo wa dawa za ALu za kutosha katika vituo vya huduma utasaidia kwa
kiasi kikubwa kupunguza vifo hivyo.
Ni
jambo la kushangaza kuona kuwa ALu zinakosekana katika vituo vingi hapa nchili
wakati kuna fedha za kutosha kutoka kwa wafadhili kwa ajili ya ununuzi wa dawa
hizo. Kwa kipindi cha miaka 10 iliyopita, Tanzania ilipokea kiasi cha dola za
Marekani 331,112,207 kutoka Global Fund pekee, ambapo kiasi cha dola za
Marekani 294,975,327 tayari zimeshatumika. Ukiachilia mbali Global fund,
malaria pia imekuwa ikifadhiliwa na Mfuko wa Ufadhili wa Rais wa Marekani (PMI
– USAID), Benki ya Dunia (World Bank) pamoja na wahisani wengine.
Yapo
makampuni makubwa manne ambayo yameteuliwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa
ajili ya kuleta dawa hizo hapa nchi. Makampuni haya yanatambulika kimataifa kwa
kuwa na uwezo mkubwa wa kuzalisha na kusambaza dawa hizo kwa vipindi maalum.
Tatizo tunaloliona hapa ni Wizara yetu kushindwa kufanya makadirio na kuagiza
dawa hizo kwa wakati.
Ni
wakati sasa kwa Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Malaria (NMCP), Bohari ya Dawa ya
Taifa (MSD), Kitengo cha Dawa cha Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii (PSS) na
Waganga Wakuu wa Wilaya (DMOs) kuchukua hatua madhubuti za kutatua tatizo la
uhaba wa Alu. Suluhu ya tatizo hili ni kwa wote wanaohusika kuwajibika kwa
dhati ili kuokoa maisha ya watanzania.
Vilevile,
tunaishauri serikali kupanua wigo wa matumizi ya mfumo wa ‘SMS for Life’ ili kuongeza dawa zingine muhimu na vifaa tiba. Mfumo
huu unasaidia sana kutoa taarifa zenye ukweli na uhalisia na kuhusu uhaba wa
dawa ili wizara ijipange kukabiliana na
tatizo hilo kwa kusambaza dawa zinazohitajika kwa wakati. Mfumo huu pia
utasaidia kwa kiasi kikubwa kuboresha uwazi na uwajibikaji katika usambazaji wa
dawa, hatimaye kuboresha utoaji wa
huduma za afya nchini.
Kwa
namna ya pekee, Sikika inavipongeza vyombo vya habari kwa juhudi zao za dhati
katika kuuhabarisha umma juu ya tatizo la uhaba wa Alu. Vyombo hivyo
vilitanguliza zaidi maslahi ya umma bila kujali matamko ya wazi ya baadhi ya
viongozi wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ya kuupindisha ukweli. Kwa mara
nyingine tena, vyombo vya habari vimeweza kuonesha uzalendo kwa kuweka maslahi
ya taifa mbele.
Mr. Irenei
Kiria, Mkurugenzi wa Sikika, S.L.P 12183 Dar es Salaam,
Simu: +255
222 666355/57, Nukushi: 2668015, Barua pepe: info@sikika.or.tz,
Twitter: @sikika1, Facebook: Sikika Tanzania, Tovuti: www.sikika.or.tz

No comments:
Post a Comment