Sikika
imesikitishwa na taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri wilayani
Kondoa ya kusitisha shughuli zake katika wilaya hiyo kupitia barua yenye
kumbukumbu namba KDC/LGC/M/3 VOL. II/71 ya tarehe 31/07/2014. Kwa mujibu wa
barua hiyo, maamuzi hayo yalitolewa katika mkutano wa Baraza la Madiwani
uliofanyika 26 Julai, 2014 Kondoa baada ya kuituhumu Sikika kwamba imesema
Madiwani hawajasoma.
Sikika inakanusha tuhuma kwamba ilisema Madiwani hawajasoma.
Maamuzi ya
kusitisha kazi za Sikika yametolewa na Halmashauri hiyo wakati shirika
likiendelea na mchakato wa kuwezesha zoezi la Ufuatiliaji
wa Uwajibikaji Jamii (Social Accountability Monitoring – SAM), zoezi ambalo
linahamasisha uwazi, uwajibikaji na utawala bora katika kusimamia rasilimali za
umma ili kuboresha utoaji wa huduma za jamii, ikiwemo afya.
Sikika inatambua kwamba serikali kuu pamoja na wafadhili hupeleka fedha
nyingi katika halmashauri zetu kwa lengo la kutoa huduma kwa wananchi, hivyo ni
jukumu la madiwani na wananchi kusimamia matumizi mazuri ya fedha hizo na
kuhakikisha huduma bora zinapatikana.
Kwa mujibu wa Kiongozi cha
Madiwani Juu ya Maswala ya Msingi na
Ujuzi juu ya Uendeshaji wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2010, Baraza la
Madiwani linawajibika kukuza ushirikiano kati ya Halmashauri, asasi za kiraia
na taasisi zingine za kiserikali. Pia, Madiwani wanawajibika kuangalia na
kudhibiti rasilimali za umma ndani ya Halmashauri zao.
Sikika inapenda kuwaeleza Watanzania kwamba inafanya kazi za SAM
katika wilaya kumi hapa Tanzania kwa ushirikiano mkubwa sana wa Madiwani
husika, na kwamba zoezi hili linakwenda vizuri na kwa mafanikio makubwa katika wilaya
tisa isipokuwa tu katika wilaya ya Kondoa, kwa sasa. Kwa mfano, Julai 2014 tumekamilisha
zoezi la SAM awamu ya pili katika Wilaya za Mpwapwa na Singida Vijijini ambapo SAM
ilifanikiwa kutokana na ushirikiano mkubwa wa Madiwani.
Sikika imeandikishwa kwa mujibu wa sheria za Tanzania kufanya kazi ya
kuhimiza utawala bora na uwajibikaji katika sekta ya afya Tanzania kupitia
uchambuzi wa sera, mikakati, mipango, bajeti na matumizi ya serikali. Majukumu
yetu ya msingi ni kuhimiza uwajibikaji katika sekta ya Afya kwa lengo la
kuharakisha upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi wote.
Kwa mantiki hiyo basi, Sikika inafanya kazi kwa karibu sana na makao
makuu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kupitia Kamati ya Huduma za Jamii tangu mwaka 2005.
Uamuzi wa kuifungia Sikika wilayani Kondoa unakiuka Kifungu cha 27(1) cha Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 kinachompa kila mwananchi wajibu wa kulinda mali asili ya Jamhuri ya
Muungano, mali ya Mamlaka ya Nchi na mali yote inayomilikiwa kwa pamoja na
wananchi.
Uamuzi huo pia umekiuka kifungu
cha 146(1) cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kinachoeleza
madhumuni ya kuwapo kwa Serikali za Mitaa kuwa ni kupeleka madaraka kwa
wananchi. Na kwamba vyombo vya Serikali za Mitaa vitakuwa na haki na mamlaka ya
kushiriki na kuwashirikisha wananchi katika mipango na shuhghuli za utekelezaji
wa maendeleo katika sehemu zao na nchini kote kwa jumla.
Tumeshangazwa kwamba barua hiyo inayozuia kazi za Sikika wilayani
Kondoa, haikueleza ni sheria gani ambayo Baraza la Madiwani limetumia kufanya
uamuzi huo na pia haikuwasilisha ushahidi wowote wa tuhuma zilizoelekezwa
Sikika.
Tumeshangazwa pia kuona kwamba Baraza la Madiwani la Wilaya ya Kondoa
linafanya uamuzi mzito kama huu kutokana na tuhuma ambazo hazijathibitishwa na
kwamba Sikika haijawahi kupewa ushahidi wowote kuhusu tuhuma hizo.
Tumeshangazwa zaidi na taarifa za Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kondoa Hamisi
Mwenda kupitia vyombo vya habari kwamba kikao cha Baraza la Madiwani kilichokaa
tarehe 26/07/2014 kufanya uamuzi huo kilihudhuriwa na madiwani 39 wakati ukweli
ni kwamba waliohudhuria ni 35. Hivyo idadi ya kura alizotangazia umma siyo za
kweli.
Sikika imesikitishwa na mwenendo wa Madiwani wa Halmashauri ya Kondoa
kuwakingia kifua watendaji wa Halmashauri kila inapojitokeza hoja inayohitaji
ufafanuzi kuhusu matumizi ya rasilimali za umma katika Idara ya Afya. Matokeo
yake, huduma za afya katika Halmashauri hiyo siyo za kuridhisha na wananchi
wanazidi kutaabika.
Sikika inaamini kwamba:
·
Uamuzi wa kusitishwa kwa
shughuli za Sikika ni moja kati ya mbinu za kuzuia zoezi la SAM awamu ya pili
lisikamilike kwani kukamilika kwake kungesababisha kuhojiwa masuala mbalimbali
ya kiutendaji, matumizi ya fedha za umma na uwajibikaji.
·
Baraza la Madiwani la
Halmashauri ya Kondoa limepotoshwa na Mkurugenzi pamoja na Mwanasheria wa Halmashauri,
na kwamba uamuzi ulifikiwa kwa kutumia maneno ya kuzusha bila ushahidi.
·
Kwamba Baraza la Madiwani la Halmashauri
ya Kondoa lina wajibu wa kusimamia watendaji wa Halmashauri na hasa Idara ya
Afya ili kuhakikisha matumizi mazuri ya fedha na rasilimali za umma kwa ajili
ya kuboresha huduma za afya wilayani hapo.
·
Kama Sikika ilichapisha
machapisho yanayohatarisha amani na usalama, taarifa na ushahidi huo
zingefikiswa kwenye kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya na uamuzi wa kamati
ungekuwa umeshawasilishwa kwa Sikika.
·
Kwamba ili kazi za SAM
ziendelee katika Halmashauri ya Kondoa kama zinavyoendelea katika Halmashauri
zingine kwa mujibu wa dhana ya utawala bora, tunasisitiza umuhimu wa uchunguzi
kufanyika ili kubaini ukweli na wapi upotoshaji umefanyika ili kutoathiri
uwajibikaji.
·
Kwamba Waziri mwenye dhamana ya
Serikali za mitaa atapata nafasi ya kufuatilia suala hili ili kujua ukweli na
kulipatia ufumbuzi kwa manufaa ya wananchi wa Kondoa.
·
Kwamba tunaisihi ofisi ya Mdhibiti
na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya ukaguzi maalumu wa fedha
(special audit) katika Idara ya Afya ya Halmashauri ya Kondoa.
·
Halmashauri ya Kondoa itajizatiti
katika kutekeleza Mpango Mkakati wa TAMISEMI wa kipindi cha 2011/12 hadi
2015/16 unaosisitiza Halmashauri za Wilaya kuzidisha ushirikiano wake na Asasi
za Kiraia katika kutimiza wajibu wa kuwahudumia wananchi.
Mwisho, tunasisitiza kwamba tuhuma kuwa Sikika ilisema madiwani wa Halmashauri
ya Kondoa hawajasoma si za kweli na hazina ushahidi. Kama upo ushahidi tupatiwe
na ujadiliwe. Pia tunasisitiza ushirikiano wetu na madiwani wote wa Halmashauri
ya Kondoa katika kusimamia rasilimali na huduma za afya Wilayani humo kwa lengo
la kuboresha huduma za afya kwa wananchi wa Kondoa.
Pili Mtambalike
Mwenyekiti wa Bodi ya Sikika.
03/8/2014
Sikika, S.L.P 12183 Dar es Salaam, Simu: +255 222 666355/57, Nukushi: 2668015, Barua pepe: info@sikika.or.tz,
Twitter: @sikika1, Facebook: Sikika Tanzania, Tovuti: www.sikika.or.tz


No comments:
Post a Comment