SIKIKA imesikitishwa na tamko
lililotolewa na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, kuhusiana na kushindwa kwa
vituo vya huduma za afya kununua dawa MSD kutokana na kuongezeka kwa deni. Ni
wazi kuwa waziri hajalipa tatizo hili uzito unaotakiwa na kutambua kuwa baadhi
ya wagonjwa wanaweza kupoteza maisha kutokana na tatizo hili.
Sikika inatambua kuwa, mapato yatokanayo
na uchangiaji katika huduma za afya ni moja tu ya vyanzo vinavyotumika katika
kuongeza upatikanaji wa dawa na vifaa tiba nchini. Na pia inatambua kuwa chanzo hiki pekee hakiwezi kuziba pengo kubwa la
ufinyu wa bajeti ya dawa na vifaa tiba muhimu ambao hauendani na mahitaji
halisi. Kwa mfano, makadirio ya mahitaji ya dawa nchini kwa mwaka wa fedha
2014/15 ni shilingi bilioni 500 lakini bajeti iliyopangwa na kupitishwa ni
shilingi bilioni 70.5 ambayo inakidhi mahitaji kwa asilimia 14 tu!
Sikika inapenda kuikumbusha Wizara ya Afya na Ustawi wa jamii kuwa,
takribani asilimia 75 ya wagonjwa
wanaopata huduma katika hospitali za Manispaa wapo katika kundi la
msamaha wa huduma za afya. Kundi hili linahusisha wajawazito, watoto chini ya
miaka mitano, wazee, watu wenye magonjwa sugu, watu wasiojiweza pamoja na watu
wenye ulemavu. Hii inamaanisha kuwa Serikali inategemea asilimia 25 tu ya
wagonjwa wanaoweza kuchangia huduma kama
chanzo kikuu cha fedha za dawa
zitokanazo na uchangiaji. Serikali inatakiwa kuwajibika katika hili na sio
kuwatupia mzigo wananchi wachache.
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii atambue kuwa, kuzitaka hospitali
kulipa deni la MSD kwa kutumia fedha za uchangiaji badala ya kutumia fedha hizo
kununua dawa kutokana na ufinyu wa bajeti, ni chanzo cha kuzifanya hospitali
hizo kuendelea kukopa zaidi na hivyo
kuendelea kukuza tatizo badala ya kutafuta suluhu. Tunamkumbusha kwamba hili ni
tatizo linalotokana mfululizo wa upangaji wa bajeti finyu kwa makusudi. Baadhi
ya hospitali hizi zimekuwa zikitumia fedha za uchangiaji kununua dawa lakini
bado zina madeni. Kwa hiyo, agizo la Waziri halitakuwa na tija katika kutatua
tatizo hili kwa sasa.
Hii sio mara ya kwanza kwa Wizara ya Afya
kuzitaka hospitali kupeleka MSD asilimia 50 ya mapato yao uchangiaji. Agizo
hili limekuwa likijirudia tangu mwaka 2012 bila ya kuwa na usimamizi katika
utekelezaji na ufuatiliaji. Kwa mfano, mwezi Julai 2014, Waziri wa Afya na
Ustawi wa Jamii aliziagiza hospitali zote kupeleka MSD asilimia 50 ya mapato
yao. Kwa kuwa agizo hili limekuwa likishindwa kutatua tatizo la upatikanaji wa
dawa, tulitarajia mbinu mbadala kutoka serikalini.
Sikika ingependa pia kujua ni jinsi gani
hospitali ya Taifa, za rufaa na maalumu ambazo zinachangia asilimia kubwa ya
deni (67%) katika kundi la madeni ya vituo vya huduma za afya zitalipa deni
hilo, kwani agizo la waziri lililenga hospitali
za wilaya na mikoa pekee. Vile
vile, tungependa kujua Wizara imeweka mipango gani katika kulipa deni lake
ambalo ni zaidi ya asilimia 70 ya deni lote ambalo MSD wanadai. Deni hilo la
Wizara linatokana na gharama za kugomboa, kuhifadhi na kusambaza bidhaa za
miradi misonge (vertical programs).
Mbali na hilo, tamko la Wizara ya Afya na
Ustawi wa Jamii kwa Umma la tarehe 27 Oktoba 2014 linaeleza kuwa, Serikali
imekuwa ikilipa Deni la MSD kwa awamu. Hata hivyo, Waziri hakuweka wazi kwamba pamoja
na kulipa kwa awamu, deni limekuwa likiongezeka kwa sababu serikali inalipa
kiwango kidogo na kukopa kiwango kikubwa. Kwa mfano, mwaka 2013 deni lilikuwa
kiasi cha Tsh. bilioni 76.4 lakini kufikia Septemba 2014 deni limekuwa na
kufikia kiasi cha Tsh. bilioni 102 ingawa serikali ilifanya malipo ya Tsh. bilioni
10 .
Sikika ingependa kupata
ufafanuzi kutoka kwa Waziri wa Afya na Naibu Waziri wa Wizara ya Fedha, Mh. Mwigulu
Nchemba ambaye hivi karibuni alinukuliwa na baadhi ya magazeti akisema kuwa
kiasi cha fedha zilizotolewa kwa ajili ya dawa katika mwaka 2013/14 ilikuwa
Tsh. bilioni 47 lakini ni Tsh. bilioni 7 tu ndizo zilitumika katika kununua
dawa. Sikika, pamoja na watanzania wote, ingependa kujua ni wapi fedha
hizi zimepelekwa na ni kwa sababu zipi hususan katika kipindi hiki cha uhaba wa dawa
na vifaa tiba katika vituo vya huduma za afya.
Sikika pia ingependa kutoa
ufafanuzi kwa umma kwamba misaada iliyositishwa na wafadhili ni kwenye bajeti
ya kuu tu (General Budget support) na
si kwenye mfuko wa pamoja wa sekta ya afya (Health
Basket Fund). Kwa kipindi cha Julai-Septemba 2014, zaidi ya Tsh bilioni 20
zilitolewa na wafadhili kwa ajili ya kusaidia halmashauri zote nchini ambapo
kwa kawaida, theluthi moja ya fedha hizo inapaswa kutumika kwa ajili ya
manununzi ya dawa na vifaa tiba muhimu.
Sikika inatambua juhudi za
serikali kujumuisha sekta ya afya katika mpango wa matokeo makubwa sasa (BRN),
ambao kwa kiasi unaweza kuchangia kupunguza uhaba sugu wa dawa na vifaa tiba katika vituo
vya huduma za afya vya umma. Hata hivyo, mpango huo utaanza kutekelezwa rasmi
mwaka wa fedha 2015/16, hivyo hauwezi kutatua tatizo la sasa la dawa. Waziri
atambue kwamba wagonjwa wanateseka na pengine baadhi kufariki kwa sababu ya
ukosefu huu wa dawa na vifaa tiba.
Mwisho, Sikika inaitaka
Wizara ya afya na Ustawi wa Jamii kuchukua hatua za haraka katika kutatua
tatizo hili sugu la ukosefu wa dawa na vifaa tiba katika vituo vya huduma za
afya vya umma. Uhaba wa dawa unawanyima wananchi kupata haki ya huduma bora za
afya ambazo huweza kusababisha vifo. Serikali inapaswa kulipa deni la MSD na
kuwezesha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kwa dharura na haraka. Sio haki kwa
serikali yoyote kuacha wananchi wake wakiteseka ama kupoteza maisha kutokanana
sababu zinazoweza kuzuilika.
Mr. Irenei Kiria, Mkurugenzi wa Sikika, S.L.P 12183 Dar es Salaam,
Simu: +255 222 666355/57, Nukushi: 2668015, Barua pepe: info@sikika.or.tz,
Twitter: @sikika1, Facebook: Sikika Tanzania, Tovuti: www.sikika.or.tz
No comments:
Post a Comment