SIKIKA imesikitishwa na taarifa za hivi karibuni zinazoeleza kuwa na
uhaba wa dawa na vifaa tiba muhimu katika vituo vya kutolea huduma vya umma
nchini. Upungufu huu unasemekana kuathiri zaidi wananchi wasio na bima za afya.
Matatizo yanayosababishwa na uhaba wa dawa ni makubwa, kwani sio tu yanatishia uhakika wa huduma kwa mgonjwa anapokuwa katika kituo cha huduma za afya lakini pia yanapunguza ari ya kufanya kazi kwa watoa huduma. Aidha, matatizo haya pia yanaathiri ustawi wa jamii na mfumo wa huduma za afya nchini. Hali hii imeathiri wananchi wengi hasa wale wasio katika mfumo wa bima za afya na wale wenye bima zenye wigo mdogo.
Nchini Tanzania, zaidi ya 80% ya
wananchi hawako katika mfumo wowote wa bima za afya na inapotokea uhaba wa dawa
na vifaa tiba wananchi hawa wamekuwa wakiathirika zaidi kwani inawalazimu
kununua dawa kwa gharama kubwa na wakati mwingine hukosa kabisa. Hali hiyo huathiri
utaratibu wa matibabu yao na kusababisha matabaka kati ya wale wasio nacho na
walio nacho kwani walio nacho wamekuwa wakipata huduma za afya.
Uhaba wa dawa na vifaa tiba muhimu
unaoendelea kwa sasa unasababishwa na ukosefu wa fedha pamoja na mlundikano wa
madeni wa baadhi ya vituo vya huduma za afya, hususani hospitali kwa Bohari Kuu
ya Dawa ya Taifa (MSD) ambao umepelekea MSD
kusimamisha kutoa huduma katika vituo hivyo mpaka pale madeni hayo
yatakapolipwa. MSD imefikia hatua hii ili kulinda mtaji wake ambao umekuwa
ukizidi kutetereka kutokana na madeni yanayozidi kulimbikizwa kutoka serikalini
pamoja na vituo vya kutolea huduma.
Baadhi ya vituo vilivyokumbwa na
kadhia ya kukosa huduma MSD ni pamoja na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili,
Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, hospitali za wilaya za Kiteto, Mpwapwa na nyingine nyingi.
Kwa mujibu wa uchunguzi wa Sikika pamoja na
vyombo vya habari, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii pekee inadaiwa na MSD
zaidi ya Tsh Bilioni 90 (Ikiwa ni gharama ya ugomboaji, uhifadhi na usambazaji
wa dawa na vifaa kutoka miradi misonge).
Aidha baadhi ya vituo vyenye
madeni MSD ni pamoja na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (8bn) hospitali ya
wilaya ya Kiteto (38Mil) na nyinginezo.
Ongezeko la deni kwa MSD limekua likiathiri ufanisi wa bohari hiyo kutokana na ukweli kuwa MSD haifanyi kazi kwa faida na mtaji wa kujiendesha yenyewe umekuwa ukipungua siku hadi siku na hivyo kupelekea MSD kushindwa kufanya manunuzi kwa wakati, kusambaza na kuwa na akiba ya kutosha ya dawa na vifaa tiba.
Ongezeko la deni kwa MSD limekua likiathiri ufanisi wa bohari hiyo kutokana na ukweli kuwa MSD haifanyi kazi kwa faida na mtaji wa kujiendesha yenyewe umekuwa ukipungua siku hadi siku na hivyo kupelekea MSD kushindwa kufanya manunuzi kwa wakati, kusambaza na kuwa na akiba ya kutosha ya dawa na vifaa tiba.
Kukua kwa deni la MSD
kunasababishwa na ufinyu wa bajeti ukilinganisha na makadirio ya mahitaji, upungufu
wa pesa inayotolewa na serikali kuu tofauti na bajeti zinazopitishwa pamoja
na ukosefu wa usimamizi na vipaumbele
juu ya matumizi ya fedha zinazotokana na uchangiaji (cost sharing).
Pamoja na
kwamba wananchi wengi huchangia pesa kutoka mfukoni, rekodi za afya zinaonesha
kuwa, mchango wake katika vyanzo vya mapato ni mdogo. Hii inachangiwa na
ukosefu wa taarifa sahihi za makusanyo na matumizi kutoka katika ngazi za
halmashauri na vituo vya huduma za afya zinazoonesha kuwa miongozo ya
ukusanyaji na matumizi ya fedha hizi haufuatwi.
Hivyo Sikika inapendekeza
yafuatayo:
● Serikali itimize ahadi yake ya kutoa fedha zote za
dawa na vifaa tiba muhimu na zitolewe kwa wakati sahihi.
● Serikali ipitie upya na kutekeleza miongozo ambayo
itatoa mwelekeo juu ya ukusanyaji na matumizi ya fedha za uchangiaji hasa fedha
za papo kwa papo. Mwongozo uliopo unasema
kwamba 67% ya ukusanyaji zitumike kwa ajili ya dawa muhimu na 15% kwa
vifaa tiba na vitendanishi lakini ni halmashauri chache sana zinazofuata mwongozo huu.
● Serikali kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii
iongeze idadi ya watu katika mfuko wa bima ya afya ili kuongeza mapato. Hii itawezesha kulipia huduma hata kwa wale
wachache watakaoshindwa kujiunga na mifuko ya bima za afya.
● Wizara ya Afya kupitia Mfuko wa Bima ya Afya wa Taifa (NHIF) iboreshe mifuko ya CHF na TIKA ili kuwawezesha wananchi kupata huduma nchi
nzima.
● Vituo vya kutolea huduma za afya na Halmashauri vinapaswa kuhakikisha kuwa makusanyo
ya fedha za uchangiaji yanatumika kwa mujibu wa miongozo, na kila wanapofanya
manunuzi ya dawa nje ya MSD wahakikishe wanapata thamani halali ya pesa.
● MSD
itimize mahitaji ya dawa kwa vituo kwa asilimia 100. Hii itavisaidia vituo
kuendelea kutoa huduma wakati wa uhaba
kwani watakuwa wanatumia akiba waliyonayo.
Mr. Irenei Kiria, Mkurugenzi wa
Sikika, S.L.P 12183 Dar es Salaam,
Simu: +255 222 666355/57, Nukushi: 2668015, Barua pepe: info@sikika.or.tz,
Twitter: @sikika1, Facebook: Sikika Tanzania, Tovuti: www.sikika.or.tz
No comments:
Post a Comment